MWENYEMACHO DOT COM

Yanapojiri Nilipo na Wewe Upo

Archive for October, 2007

KARIBU MKUTANO MKUBWA WA WASHAIRI 3/11/2007

Posted by Bob Sankofa on October 31, 2007

washairi.jpg

Kuna kitu tuligundua jana kwenye mkutano wa malenga wa bongo, ni kwamba watu wakikaa sakafuni wanapata mzuka zaidi wa kughani kuliko wakiketi kwenye viti. Basi jana jumuiya nzima tuliketi sakafuni, tukaghani mashairi yetu, tukanywa mvinyo, tukala piza halafu tukatangaziwa kuwa siku ya jumamosi ya tarehe 3/11/2007, kilabu chetu cha ushairi kinatimiza miaka miwili tangu kuanzishwa kwake kwa hiyo kutaangushwa bonge la pati pale Alliance Francaise. Kwa habari zaidi bofya hapa. Pia siku si nyingi A Novel Idea wanafungua duka kubwa zaidi la vitabu pale Shoppers Plaza, tutahamia huko kwa ajili ya nafasi ya kutosha. Karibuni kwa kila kitu 🙂

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Fotografia, Mikutano, Photography, Poetry, Sanaa, Tanzania, Ushairi | 3 Comments »

KUNA ZAIDI YA USHAIRI

Posted by Bob Sankofa on October 31, 2007

washairi-2.jpg

Kwenye makutano ya washairi wa bongo jana kulikuwa na zaidi ya ushairi na mvinyo, tulipata bahati ya kutembelewa na mwanachama mpya, dada Tatu, yeye ni mwanamziki na mshairi kwa pamoja. Alitutumbiza kwa kibao murua cha Malaika. Unaweza kumuona Erick (Mzungu hapo kulia) jinsi alivyochotwa na upigaji gita na uimbaji wa dada Tatu, dada Clara Swai (pale kushoto) yeye hakusita kuserebuka kabisa. Kila mwezi kuna wanachama wapya wanaongezeka na kuna vitu vipya vinaongezeka, Fanani Flava inazidi kuboreka. Karibu na wewe tuone kipaji chako.

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Mikutano, Photography, Poetry, Sanaa, Tanzania, Ushairi | Leave a Comment »

WASHAIRI WA BONGO WAKUTANA TENA

Posted by Bob Sankofa on October 31, 2007

washairi-3.jpg

Jana, tarehe 30, ilikuwa ni jumanne ya mwisho wa mwezi huu wa kumi. Kama ilivyo ada jumanne ya mwisho wa mwezi huwa ni siku maalum kabisa kwa wanajumuiya ya ushairi hapa bongo (Fanani Flava) kukutana na kusikilizishana tungo zao za mwezi huo. Makutano yalikuwa ni pale pale pa siku zote, duka la vitabu la A Novel Idea, kule slipway. Pichani ni baadhi ya washairi wakisubiri kuingia ndani kughani tungo zao.

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Mikutano, Photography, Poetry, Sanaa, Tanzania, Ushairi | Leave a Comment »

MANYANI NANI TAMASHANI

Posted by Bob Sankofa on October 29, 2007

manyani-band.jpg

Majira ya jioni jioni hivi katika siku ile ya Ijumaa ambayo nilihudhuria tamasha, wakapanda jamaa wa bendi ya Manyani Nani. Jamaa maskani yao ni Bongo Darisalama. Kwa kifupi ni kuwa hawa jamaa ni funga kazi, wanatwanga saundi la kimataifa kabisa. Kwa saundi lao waliweza kusimamisha shunguli za mji wa Bagamoyo kwa muda wa saa nzima ili kuwasikiliza. Hii unayoona hapa ni sehemu tu ya nyomi lililokuwa likishuhudia shughuli waliyokuwa wanaitoa jamaa

manyani-band2.jpg

Picha hii ni kwa mbele ya bendi ya Manyani Nani. Huyo mwenye gitaa hapo mbele ni Paul Ndunguru, mwimbaji kiongozi wa bendi, dada katikati hapo ni Tishi, mneguaji, halafu kuna kaka kwenye ngoma kule nyuma ni Fujo. Na yule mwenye gitaa, ambaye sura yake haionekani ni Freddy Saganda. Hawa ni baadhi ya wanaounda kundi hili la Manyani Nani Band.

Baada ya onesho la hawa jamaa nikajipandia zangu “kipanya” (usafiri wa umma) kurejea zangu jijini.

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Photography, Sanaa, Tanzania | Leave a Comment »

WENYEJI – TAMASHA LA SANAA

Posted by Bob Sankofa on October 29, 2007

wabagamoyo.jpg

Hawa ni jamaa wa kundi la PKK la Bagamoyo, wenyeji wetu hawa. Jamaa matata sana katika swala zima la kutawala jukwaa. Ni wanamuziki wa kiasili. Wanachanganya vyombo vya kisasa vya muziki ili kuongeza ladha katika muziki wa nyumbani. Wanapiga mirindimo ya ngoma mbalimbali za Kiafrika, yani tangu kusini hadi Kaskazini halafu Mashariki hadi Magharibi mwa bara hili.

Hapa wanalisakanyua jukwaa kwa mtindo wa ngoma ya asili iitwayo Malivata. Kilichonifurahisha hapa ni kuwa katika muda huu ambao wanacheza hapa palikuwa hakuna chombo kinachopigwa na bado watu walikuwa wakishangilia hakuna mfano. Baada ya onesho lao wakaniambia eti hii ilikuwa ni mara yao ya kwanza kabisa kupanda kwenye jukwaa, sikuamini kwani kazi waliyofanya ni ya kiufundi mno. Poa sana hawa jamaa.

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Photography, Sanaa, Tanzania | Leave a Comment »

SANAA MBADALA

Posted by Bob Sankofa on October 29, 2007

maonesho.jpg

Kuna wakati fulani katika Tamasha hili la sanaa la 26 kwenye jukwaa yalikuwa yakipanda makundi fulani ya uimbaji au maigizo. Makundi yale kwa kweli yalikuwa hayana mvuto sana, nafikiri ilitokana na ufinyu wa kujipanga sawaswa au ni ukosefu wa uzoefu wa kukutana na hadhira kubwa yenye mshawasha wa kupindukia juu ya sanaa. Basi ilikuwa ukikereka kama mimi uanapata nafasi ya kwenda kuona sanaa mbadala.

Hii ndio hasa raha ya Tamasha la Sanaa la Bagamoyo, kila sehemu kuna kitu fulani kinaendelea. Kwa mfano hapa watu wanapita katika mabanda yenye sanaa za vinyago, picha na mitindo ya nguo. Ukipenda sanaa zile mbadala unawaunga mkono wabunifu wa sanaa zile. Nimenunua shati la ‘kirasta’ na gauni kwa ajili ya binti malkia wa roho yangu hapa.

Posted in Africa, Art, Biashara, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Kazi, Photography, Sanaa, Tanzania | Leave a Comment »

NGOMA

Posted by Bob Sankofa on October 29, 2007

ngoma.jpg

Hawa ni wacheza ngoma wa kikundi cha Jijini Dar es Salaam wakionyesha manjonjo katika Tamasha la 26 la Sanaa pale Bagamoyo. Kundi hili ni kati ya machache ambayo yaliturusha roho kisawasawa kwa umaahiri wao wa kunengua miondoko ya ngoma za asili. Walitoa burudani kwa saa nzima bila kupumzika na walipomaliza Bagamoyo nzima wakataka waendelee kidogo ila kama unavyojua tena, mambo ya itifaki, tukaambiwa eti ratiba haituruhusu, muda umetutupa mkono. Basi wakajiondokea zao. Nasikia walitimua tena vumbi siku ya Jumamosi usiku, sikufanikiwa kuwaon kwani nilikuwa nakimbiza maswala mengine DSM.

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Photography, Sanaa, Tanzania | Leave a Comment »

TAMASHA LA 26 LA SANAA BAGAMOYO

Posted by Bob Sankofa on October 29, 2007

tamasha.jpg

Juma lililoisha pale Bagamoyo kulikuwa na tamasha kubwa la sanaa. Tamasha lile lilidumu kwa siku sita mfululizo, yani lilianza siku ya Jumatatu hadi Jumamosi iliyopita. Nilifanikiwa kwenda siku ya Ijumaa. Tamasha hili lilikuwa ni la 26 kufanyika katika Chuo cha Sanaa pale Bagamoyo. Tamasha hili hubadili kabisa mandhari ya Bagamoyo kwa siku chache kabisa. Bagamoyo ni mji mdogo sana na maisha yake ni ya mwendo wa taratibu lakini punde mbiu ya Tamasha inapolia huwa Bagamoyo haina kulala. Ni mirindimo ya muziki wa asili na muziki wa sasa, ngoma, ushairi, maigizo na mambo kadha wa kadha.

Tamasha hili si la kwanza mimi kuhudhuria, kwa tathmini ya haraka naweza kusema Tamasha la mwaka huu halikunivutia sana, lilipooza. Kwa nini? Sina jibu la moja kwa moja lakini nadhani sababu ya msingi kabisa ni kuwa maonesho yalikuwa yakifanyika katika ukumbi finyu sana (Jukwaa la mwebeni), ukumbi rasmi uliungua na moto na sasa ndio unapigwa ukarabati. Labda mwakani mambo yatakuwa ‘bye’ zaidi.

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Photography, Sanaa, Tanzania | Leave a Comment »

TOKA RHYMSON NA KWANZA UNIT HADI ZAVARA, KULIKONI?

Posted by Bob Sankofa on October 25, 2007

ramson.jpgramson.jpg

Kwanza nitangulize samahani kwa kuwatelekeza wadau wangu kwa kitambo kidogo. Niliwatelekeza kwa mema wala si kwa shubiri. Nilikuwa katika mchakamchaka wa kuhakikisha blogu inakuwa na ladha zaidi. Muda si mfupi utagundua kuwa blogu yetu tangu sasa itakuwa si tu ya MWENYE MACHO tu bali pia MWENYE MASIKIO.

Tangu sasa blogu itakuwa ikikuletea mahojiano ya sauti yani podikasti, na mahojiano yetu yamefanikiwa kuanza na mkongwe wa Muziki wa Hip Hop hapa Tanzania, naye si mwingine bali ni Rhymson. Utakumbuka kuwa Rhymson na kundi lake la Kwanza Unit au KU CREW, aliweza kuwa msanii wa mwanzo kabisa wa muziki wa Hip Hop kutokea na kundi lake katika luninga.

Katika mahojiano haya naongea na Rhymson ambaye sasa ametwaa jina la Kiafrika na kuitwa Zavara Mponjika. Anatueleza ni kwa nini aliamua kutwaa jina la Kiafrika na kuachana na jina lake la awali ambalo yeye analiita la kikoloni. Pia anatufafanulia iwapo yeye ni mfuasi wa imani ya Rastafarian ama lah, yote hii ni kutokana na maisha anayoishi baada ya “kuzaliwa upya”, na hasa swala zima la kuwa na nywele msokoto.

Zavara pia anaongea nami kuhusu maisha yake kule ughaibuni (Canada) ambako alikaa kwa takribani miaka kumi. Je unafahamu kuwa Zavara alikuwa akitengeneza filamu, lakini uajua kuwa alikuwa akitengeneza filamu hata kabla ya kwenda ughaibuni? Sikiliza mahojiano haya halafu utafahamu ameshiriki kutengeneza filamu ipi na ipi pamoja na tamthilia za luninga kama “Earth, the Final Conflict” ambazo zimewika sana huko ughaibuni, na pia ni wanafilamu gani wengine ambao alifanya nao kazi na wameendelea kuwa maarufu kabisa katika soko la filamu.

Zavara anazungumzia muziki wa kufokafoka (Hip Hop) waliokuwa  wakipiga enzi zao na anaulinganisha na huu wa sasa na kutoa mawazo yake. Sikiliza amesema nini. Anazungumzia video ya Kwanza Unit ya “We Run Tingz” ambayo aliiongoza katika upigaji wake wa picha miaka ile ya 90. Anaeleza ni kwa nini video ile kongwe bado inapendwa na kuoneshwa sana na vituo vya televisheni vya hapa nyumbani japo haikuwa na wakina dada wakata viuno wala watu waliovaa minyororo shingoni. Anaeleza alijifunza wapi kutengeneza sinema wakati miaka hiyo akifanya kazi zake Tanzania ilikuwa haina hata shule moja ya filamu.

Katika mahojiano haya ya dakika takribani 39 na ushee, Zavara pia anazungumzia Mradi wa WAPI. Anatueleza WAPI ni nini na wazo la mradi ule alilipata vipi. Anaeleza ni kwa jinsi gani mradi umekua kwa haraka sana bila hata ya kuutangaza katika vituo vikubwa vya habari na bila ya kutumia pesa nyingi.

Fuatana nami, Bob Sankofa, katika mahojiano haya ya kwanza kabisa katika blogu hii. Tafadhali bonyeza hapo chini kusikiliza.

[odeo=http://odeo.com/audio/17193323/view]

Iwapo utapenda kuyaweka mahojiano haya kwenye blogu yako tafadhali usisite kufanya hivyo. Pia iwapo utapenda “kuyashusha” yani ku-download na kuyaweka kwenye simu yako ya mkononi au iPod au kuyahifadhi kwenye CD ili usikilize kwenye radio yako baadae bonyeza hapa. Mahojiano haya yanatakiwa kusambazwa bure kabisa bila kutoza fedha yeyote.

Naomba nikukimbie kwa sasa, naelekea Bagamoyo kwenye tamasha la sanaa ambalo limeanza tangu Jumatatu ya wiki hii, linakwisha keshokutwa. Pia usisahau kuwa utamaduni wa WAPI unafanyika tena Jumamosi ijayo pale British Council na mgeni wetu atakuwa Mama Maria Shaba.

Hadi wakati mwingine,

UHURU!

Picha na Podikasti: Bob Sankofa

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Filamu, Fotografia, Kazi, Kimataifa, Photography, Podikasti, Poetry, Sanaa, Tanzania | 6 Comments »

30th OCTOBER POETRY NITE – LAST TUESDAY OF THE MONTH‏

Posted by Bob Sankofa on October 20, 2007

poetry.pngPoetry nite is here once more. We meet on Tuesday 30rd Oct 2007, from 19H00 at A Novel Idea Slipway. Theme for the nite is “Celebration”, cos we are celebrating the club’s 2nd anniversary. Please read to the very end.
 
COME TO POETRY NITE
“Come one, come all,
Come read, or discuss,
the magical bliss,
of poetry’s kiss…
 
Come grab and munch,
Sip on wine or punch,
while we sit in a bunch,
on a big round couch…
 
All faces are happy,
broad and shiny,
lovely and ready,
To knock down poetry…
 
all the same thou,
if I were you Lou?,
Or Lisa Patlou?,
I wouldnt miss out,
on poetry nite…”
 
by Clara Swai
 

 

 

 

 

 

 

* Reminding each member to contribute TShs. 3,500/= for refreshments and drinks.
* Also visit our blog at http://fananiflava.blogspot.com for more insight into what we are all about.
* Mucho gracias to “A Novel Idea” staff and management, for sharing their space and time with us all. We continue to enjoy the 10% discount on any book purchase

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Mikutano, Photography, Poetry, Sanaa, Tanzania, Ushairi | 1 Comment »

LUCKY DUBE AFARIKI DUNIA

Posted by Bob Sankofa on October 19, 2007

lucky-dube.jpg

Lucky Dube, mwanamuziki maarufu wa mtindo wa reggae, amefariki dunia Jo’berg, Afrika ya Kusini kwa kupigwa risasi siku ya Alhamisi ya tarehe 18 Oktoba, 2007. mauaji hayo yalitokea katika kitongoji cha Rosettenville ambako wauaji wake walitaka kumpora gari yake na hatimaye kuishia kumpiga risasi na kumuua, Polisi wa hapa wamesema.

Dube, alizaliwa  Johannesburg Agosti 3, 1964. Amefariki akiwa na umri wa miaka 43. Aliwahi kurekodi album karibu 20 hivi, zikiwemo Rastas Never Die, Think about the Children, Soul Taker na Trinity. Albamu yake mpya kabisa ni ile aliyoitoa 2006, ambayo aliita Respect. Dube alikuwa na mashabiki kibao nyumbani na duniani kote pia.

Watu wengi walipata taabu sana kumtambulisha Dube kama Rastafarian wa “kweli”, yeye mwenyewe alipokuwa akiulizwa alikuwa akisema, “Kama kuwa rasta maana yake ni kufuga nywele msokoto, kuvuta bangi na kuamini kwamba Haile Sellasie ni Mungu basi mimi si Rastafarian lakini iwapo Urastafari ni njia ya kujikomboa kisiasa, kijamii na kimawazo basi mimi ndiye.”

Inasemekana kuwa mtu aliyechangia sana kwa Dube kupiga muziki wa Reggae ni Peter Tosh, amabye naye aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka 1989. Dube anasema mirindimo ya Tosh ndiyo hasa aliyojifunza kwayo lakini bado anakubali kuwa Bob Marley ndiye hasa mfalme wa miondoko ya Reggae duniani. Anasema, “Isingekuwa Bob labda tusingeifahamu reggae duniani kama tunavyoifahamu leo.”

Ni kitu cha kustaajabisha na kusikitisha kwa kuona ni kwa namna gani mwanadamu anazidi kuwa mnyama siku baada ya siku. Sote tutakufa siku moja lakini kifo cha Dube, ambaye alichangia kwa kiasi fulani kufanya watu wa rangi tofauti kuweza kuishi kwa kusikilizana pale Kusini, ni sawa na shukrani ya punda ambayo mara nyingi huwa ni mateke. Miziki yake siku zote ilisimamia heri, wamechukua roho yake kwa shari.

Jah amlaze mahala pema peponi Ras Luck Dube.

Posted in Africa, Art, Burudani, Kazi, Kimataifa, Poetry, Sanaa, Ushairi | 5 Comments »

CHONDE CHONDE, USIACHE KUJA!

Posted by Bob Sankofa on October 17, 2007

dance.jpg

MIONZI DANCE THEATRE

Inakuletea

VISA 2 DANCE FESTIVAL

SIKU: Ijumaa, 19 Oktoba 2007

MAHALI: Russian Culture Centre

MUDA: Kuanzia Saa moja Kamili ya Jioni

KIINGILIO: Bure ila unaruhusiwa kuchangia mwisho wa tamasha

MAONESHO:

1. MANENO YA NGOMA italetwa kwako na FUJO (music solo) na wanafunzi wake
Muda: 10 minutes

2.THE EGG, ni ngoma iliyotayarishwa na kuchezwa na Aloyce Makonde
Muda: 20 Minutes

3.CHIBITE, ni muziki uliotayarishwa na kuchezwa na Andrea Kalima Zawose kutoka Bagamoyo
Muda: 10 minute

4.UPSIDE DOWN ngoma iliyotayarishwa na kuchezwa na Ian Mwaisunga
Muda: 15 minutes

NA MENGINEYO MENGI,

USIACHE KUJA, MWAMBIE NA RAFIKI YAKO!

Picha kwa Msaada wa Google Search

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Fotografia, Kazi, Photography, Sanaa, Tanzania | Leave a Comment »

TUMKUMBUKEJE MWALIMU? – JOHN POMBE MAGUFULI

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

065.JPG

Baada ya Profesa Shivji kushangiliwa sana kutokana na mawazo yake aliyoyatoa katika kumuenzi Mwalimu, John Magufuli, Waziri wako wa Ardhi, akaona ngoja apimane nae nguvu kidogo. Akapanda na kukamata kipaza. 

Anashangiliwa, jumuiya ya Chuo Kikuu inaonekana kumpenda sana huyu jamaa sijui kwa nini, labda kwa sababu kila mwaka lazima aje, au labda ni kwa sababu naye ni mwanafunzi hapa. Anatuambia toka mwaka jana anasomea Kemia hapa chuoni. Alah! Hata mie nilikuwa sifahamu hilo. 

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Bongo, Elimu, Fotografia, Mikutano, Photography, Siasa, Tanzania | Tagged: , , , , , , , , , | Leave a Comment »

PROFESA ISSA SHIVJI ALIVYOMKUMBUKA MWALIMU

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

062.JPG

Tumerudi kwenye ngwe ya pili ya kumjadili Mwalimu baada ya mapumziko mafupi. Wa kwanza anayepewa nafasi ya kumzungumzia Mwalimu kwa sasa ni mhadhiri wa Sheria wa siku nyingi, Profesa Issa Shivji. Shivji pia ni mmoja wa Wajamaa wachache waliosalia wanaoishi katika jamii ya kibepari. Kwa wale wenye tatizo na Richa Adhia, mrembo wa Tanzania 2007, nadhani watakuwa na tatizo pia na uhalali wa u-Tanzania wa mhadhiri huyu. Haituhushu kwa sasa tuendelee. 

Katika kumjadili Mwalimu, Shivji anaanza kwa kusema, “Huu si tu mwaka wa 8 toka Mwalimu kufariki bali pia ni mwaka wa 40 tangu kuzaliwa kwa Azimio la Arusha. Mbona wote tumesahau basi kukumbuka kuuawa pia kwa Azimio? Hata Taasisi ya Mwalimu pia imesahau hilo, ingekumbuka ingetutahadharisha katika kutengezeza kauli mbiu ya kumkumbuka Mwalimu na marehemu mwanae, Azimio la Arusha.” 

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Bongo, Elimu, Fotografia, Mikutano, Photography, Siasa, Tanzania | Tagged: | Leave a Comment »

PROFESA BAREGU NA MWALIMU NA UMOJA WA AFRIKA

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

053.JPG

Profesa Baregu ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika masuala ya Siasa na Jamii. Na yeye kama walivyokuwa watoa mada wengine anapewa dakika thelathini ili azungumzie mchango wa Mwalimu katika suala zima la kuwa na Afrika iliyo moja. 

Profesa Baregu mwenyewe hayuko hapa ukumbini, tunaambiwa amekwenda kwenye msiba huko Bukoba. Lakini amekataa katakata kuleta ile samahani yetu tuliyoizoea, “Samahani sikuweza kufika wa sababu zisizoweza kuzuilika”. Baregu amemtuma Bashiru Ali, mhadhiri msaidizi hapa Chuoni, kutoa hotuba kwa niaba yake. Hapajaharibika kitu, hebu tusikilize Profesa alikuwa ameandaa nini. 

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Bongo, Elimu, Fotografia, Mikutano, Photography, Siasa, Tanzania | 1 Comment »

PROFESA ESTARIA BHALUSESA NA MWALIMU NA ELIMU

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

051.JPG

Baada ya Jenerali ambaye hotuba yake ilipigiwa makofi kwa dakika mbili nzima, sasa anapanda Profesa wa masuala ya Elimu hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Estaria Bhalusesa. Anaomba watu wamuwie radhi kwani hotuba yake aliianda kwa lugha ya kikoloni (Kiingereza), panapita ukimya mfupi, halafu naanza kusikia sauti za baadhi ya viti vikisogezwa na baadhi ya watu wanaanza kutoka nje ya ukumbi huu wa Nkrumah.

Najaribu kusikiliza anachoongea, hotuba yake ina mantiki kubwa sana, lakini amekosea sana kutuletea hotuba hii kwa kimombo wakati wahudhuriaji hapa asilimia 99.9 tunazungumza kiswahili. Naona kuna wazungu na waasia hapa na pale. Nafikiri Profesa amejifunza kitu hapa. 

Read the rest of this entry »

Posted in Bongo, Elimu, Fotografia, Kimataifa, Mikutano, Photography, Siasa, Tanzania, Uncategorized | Leave a Comment »

JENERALI ULIMWENGU NA KAZI ZA MWALIMU

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

035.JPG

Jenerali Ulimwengu anapewa nafasi ya kuzungumzia kazi za Mwalimu Nyerere. Anaanza kwa kusema huwezi kuzungumzia kazi za Mwalimu katika muda wa dakika thelathini ambazo waratibu wa kumbukumbu hii wamempatia. Anasema atakachozungumzia yeye ni kama dibaji tu ya kazi za Mwalimu. 

Anaanza kwa kusema kuwa ukitaka kuzungumzia kazi za Mwalimu ni lazima kichwani kwako uelewe kuwa Mwalimu alikuwa ni mtu mwenye kupenda kubadilika, anasema hadi Mwalimu anafariki katika umri wake mkubwa aliokuwa nao, akili yake bado iliweza kufikiri kileo. Anatoa mfano kuwa wakati kuna watu wengi ndani ya CCM, ambacho kilikuwa ni chama cha Mwalimu hadi mauti yanamkumba, kilikuwa kikipinga kabisa kabisa ujio wa sera ya vyama vingi, Mwalimu hakuona aibu kusimamia kidete ujio wa mabadiliko yale kwani alikwishaona wimbi la mabadiliko yaliyokuwa yakitokea ulimwenguni. Jenerali anasema kuwa, “Usisahau kuwa Mwalimu alikuwa ni kiongozi wa kwanza kufutilia mbali mfumo wa vyama vingi hapa nyumbani lakini muda wake ulipopita hakuona haya kusema kuwa jitayarisheni kwa mabadiliko.” 

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Bongo, Elimu, Fotografia, Photography, Siasa, Tanzania | 3 Comments »

NANI ALIKUWEPO KUMKUMBUKA MWALIMU?

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

salim.JPG

Dakta Salim Ahmed Salimu, aliyewahi kuwa katibu mkuu wa OAU na sasa mwenyekiti (kama sijakosea) wa Taasis ya Mwalimu Nyerere alikwepo kumuenzi Mwalimu. Kumbuka Salim aliwahi kupewa kazi ya kuliwakilisha taifa kimataifa angali kijana mdogo kabisa wa miaka kumi na tisa tu. Pembeni ya Dakta Salim ni balozi wa Afrika ya Kusini, kumbuka pia kuwa Afrika Kusini ina deni kubwa sana la fadhila kwa Tanzania kutokana na msaada wa hali na mali Tanzania iliyoipatia Afrika ya Kusini kipindi kile cha vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, ndio maana balozi yuko hapa.

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Bongo, Elimu, Fotografia, Kazi, Mikutano, Photography, Siasa, Tanzania | Leave a Comment »

MWAKA WA NANE, MWALIMU BADO AKUMBUKWA VYEMA.

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

009.JPG

Kila tarehe 14/10 wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hujumuika na Watanzania wengine kote nchini kumkumbuka muasis wa taifa la Tanzania, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Maadhimisho ya mwaka huu yalikuwa ni ya nane tangu Mwalimu kututoka. Kama ilivyo ada mwaka huu pia watu wamekusanyika tena katika ukumbi maarufu wa Nkrumah pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutimiza azma yao. 

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Bongo, Elimu, Fotografia, Mikutano, Photography, Siasa, Tanzania | Leave a Comment »

WAPI YA SEPTEMBER – WANAMAPINDUZI SOKONI

Posted by Bob Sankofa on October 11, 2007

wanamapinduzi.JPG

Wiki hii, kule nchini Argentina ni wiki ya kumkumbuka mwanamapinduzi, Che Guevara. Nikawa naangalia kwenye CNN watu wanamzungumziaje Che, mzaliwa wa Argentina. Rafiki yake wa karibu sana, wakati wa utoto wao, akasema “Che akifufuka leo anaweza asiamini watu wanavyoifanyia biashara sura yake na kujipatia faida lukuki, kitu ambacho Che mwenyewe alikuwa akikipinga hadi mauti yake”.

Mwingine akasema, “Walipomuua walidhani wameua na mwazo yake pia, lakini ukweli ni kuwa Che yu hai hata baada ya miaka 40 ya kifo chake na kwa kumuenzi tunamvaa vifuani mwetu hata sasa”.

Kwenye WAPI huwa kuna jukwaa la wabunifu wa mitindo ya mavazi, King’oko, ambao wanapatiwa fursa ya kuhakikisha kila muhudhuriaji wa WAPI ananunua walau taswira moja ya wanamapinduzi ampendaye, kuna Che kwa juu pale, Samora katikati na Lumumba kwa chini. We unaionaje hiyo?

Picha na: Bob Sankofa

Mahali: British Council

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Fotografia, Mikutano, Photography, Siasa, Teknolojia | 3 Comments »

WAPI YA SEPTEMBER – MUZIKI MKONGWE

Posted by Bob Sankofa on October 11, 2007

wanangoma.JPG

Wenye akili zao karibu wote waliowahi kuishi hapa duniani waliwahi kusema, “Kabla hujasifia utamaduni wa mwenzio fahamu ya kuwa na wewe una wa kwako, na usipoutukuza wa kwako katu hakuna atakayekutukuza.”

WAPI katika mwezi huu wa tisa wakautilia maanani msemo huo hapo juu. Wakazama ‘master bedroom’ ya nyumba ya Jakaya, Dodoma kwenyewe. Kufumba na kufumbua wakashuka na hivi vifaa, jamaa ni mwendo wa mazeze, marimba za mkono na sauti zao za asili lakini ukisikiliza kwa makini wanapiga mirindimo ya hip hop kabisa.

Kwa mantiki hiyo basi watu wana kila haki ya kuubatiza mziki wa sasa jina la “Muziki wa Kizazi Kipya” kwani ni kweli kabisa kuwa “Muziki Mkongwe” ungalipo hata sasa.

Picha na: Bob Sankofa

Mahali: British Council

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Fotografia, Kazi, Mikutano, Photography, Poetry, Sanaa, Siasa, Tanzania, Ushairi | Leave a Comment »

WAPI YA SEPTEMBER – HIP HOP HALISI

Posted by Bob Sankofa on October 11, 2007

kizazi-kipya.JPG

Kuna watu wana hasira na mfumo wa mambo ulivyo hivi sasa. Kuna watu kibao wamekuwa wakifanya mambo makubwa kupindukia lakini wamekuwa wakiambiwa kuwa ukitaka kusikika basi “kula nao”. Wamegoma kunywa ‘mvinyo’ wao wa ufisadi na kazi zao zimeshindwa kupigwa kwenye radio ‘zao’ hao mafisadi.

Utamaduni wa WAPI umewagundua watu hawa na umewapa jukwaa la kusema yaliyo mioyoni mwao. Hawa ni wale vijana wanaoitwa “Undergrounds”, hawawezi kuwa maarufu kwa sababu hawana pesa ya kumuhonga DJ ili nyimbo zao zichezwe radioni. Hutakaa uwasikie huko uliko, lakini wana jambo wanataka kusema na wanalisemea pale kwenye utamaduni wa WAPI.

Nyimbo zao hutaweza kuzisikia kwa sababu zinaongea ukweli, wamegoma kuwachezesha dada zao nusu uchi kwenye video, wanakomaa na hip hop halisi.

Picha na: Bob Sankofa

Mahali: British Council

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Mikutano, Photography, Poetry, Sanaa, Siasa, Tanzania, Ushairi | Leave a Comment »

WAPI YA SEPTEMBER – GRAFITI

Posted by Bob Sankofa on October 11, 2007

haribu-ukuta.JPG

Katika shughuli nzima ya utamaduni wa WAPI, ambao hufanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, watoto wa Jakaya (Watanzania) huwa wanapewa fursa ya kuonyesha vipaji vyao vya uchoraji wa grafiti ukutani. British Council hutoa ukuta wake bure pamoja na makopo ya rangi ili ukuta wake ‘uchafuliwe’ na vijana wa Jakaya.

haribu-ukuta2.JPG

Katika kuta zile vijana wa Jakaya hutakiwa kuelezea kauli mbiu ya mwezi ya WAPI kwa kutumia rangi zile, kauli mbiu ya September ilikuwa ni “Amani Tanzania, Baraka au Laana?”. Zile rangi ni bei aghali sana kwa mtu wa kawaida kuweza kumudu, kopo moja huuzwa shilingi 3,000 hadi 7,000 kutegemeana na ubora wa rangi. British Council wanatumia fedha zao kuhakikisha vijana wa Jakaya wanapata rangi. Kazi hii ya grafiti inakuhitaji kila baada ya mchoro pia ukapate maziwa ya kutosha maana rangi zile zina harufu kali sana.

Picha na: Bob Sankofa

Mahali: British Council

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Fotografia, Kazi, Mikutano, Photography, Sanaa, Siasa, Tanzania | 1 Comment »

MRISHO MPOTO, MWANAMAPINDUZI!

Posted by Bob Sankofa on October 11, 2007

mpoto-2.JPG

Pengine Mrisho Mpoto ndiye mshairi pekee katika Tanzania nzima ambaye anaishi kwa kutegemea sanaa pekee. Mrisho ni msanii wa ushairi, anafanya ushairi wa Kiswahili. Mara yangu ya kwanza kabisa kuweza kuongea na Mrisho ana kwa ana nakumbuka ilikuwa ni mwaka 2005, tulikutana pale kijiji cha Makumbusho. Sikumbuki sawasawa kulikuwa na shughuli gani pale ila nakumbuka kuwa siku ile ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kukutana na Mrisho.

Nakumbuka katika mazungumzo yetu mafupi neno “Kaka” ndilo neno alilolitaja mara nyingi katika sentensi zake. Kabla hata ya kukutana na Mrisho macho kwa macho nilikwishazisikia sifa zake hapo awali na nilikwishawahi kumuona pia kwenye igizo la “Mfalme Juha” lililoandaliwa na kikundi chake cha Parapanda, pale Russian Cultural Hall, mwaka 2003. Mrisho alicheza kama Mfalme Juha siku ile na kwa mara ya kwanza niliiona hadithi ile ya bwana Farouk Toupan ikiishi.

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Art, Blogu za Kiswahili, Bongo, Burudani, Elimu, Fotografia, Kazi, Mikutano, Photography, Poetry, Sanaa, Siasa, Tanzania, Teknolojia, Ushairi | 3 Comments »

MWANAFALSAFA “AFARIKI DUNIA”

Posted by Bob Sankofa on October 5, 2007

mwana.jpg

Hiyo ndiyo habari iliyokuwa imezagaa jijini kote usiku wa Jumanne na mchana mzima wa Jumatano ya wiki hii.

Mimi binafsi niliipata habari hiyo nikiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere, kumsindikiza rafiki. Nilikuwa nikiendesha gari ikabidi nilipaki pembeni na kuongeza sauti ya radio ili kusikiliza vizuri habari ile. Niliipata habari ile kupitia radio Clouds FM, lakini muda huohuo “The People’s Station” haikuchelewa kumsaka Mwana FA mwenyewe na kumweka hewani kwa njia ya simu kukanusha habari hizo.

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Fotografia, Kazi, Photography, Poetry, Sanaa, Tanzania, Ushairi, Vijimambo | 10 Comments »

SANKOFA USHAFIKA KWA “BIBI”?

Posted by Bob Sankofa on October 5, 2007

bobby.jpg

“Sankofa ati uko ulaya tayari?”

Nimeulizwa swali hili karibu na kila mdau wa blogu hii kupitia barua pepe.

Ukweli ni kuwa ilikuwa niwe kwa “bibi” (Uingereza) tangu tarehe 30 ya mwezi uliopita lakini kidogo wenyeji wangu, Nollywood Entertainment Limited, ni Wanaijeria hawa, wameendeleza libenenge lao la kutotimiza ahadi zao. Wanaleta siasa kwenye sanaa.

Read the rest of this entry »

Posted in Africa, Art, Filamu, Sanaa, Tanzania, Vijimambo | 8 Comments »

SHUKRANI – TUENDELEE KUPIGA KURA

Posted by Bob Sankofa on October 1, 2007

Nawashukuruni sana wadau kwa kupiga kura kwa moyo wote. Hatimaye hadi sasa PLAY YOUR PART inaongoza. Hii ni kwa juhudi zenu. Asanteni sana. Naomba tuendelee kupiga kura zaidi na zaidi kwani jamaa zetu wa Zambia hawajalala, wanakuja kwa kasi.

Niko haihai kidogo, nitawasiliana nanyi baadae kidogo.

Kuna filamu nyingine ya Kitanzania, FIMBO YA BABA, nayo inafanya vizuri kwa kura, inaongoza. Tafadhali endeleeni kuzipiga kura PLAY YOUR PART na FIMBO YA BABA.

UHURU!

Posted in Africa, Art, Bongo, Burudani, Elimu, Filamu, Fotografia, Kazi, Kimataifa, Photography, Sanaa, Tanzania, Teknolojia | Leave a Comment »