MWENYEMACHO DOT COM

Yanapojiri Nilipo na Wewe Upo

JENERALI ULIMWENGU NA KAZI ZA MWALIMU

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

035.JPG

Jenerali Ulimwengu anapewa nafasi ya kuzungumzia kazi za Mwalimu Nyerere. Anaanza kwa kusema huwezi kuzungumzia kazi za Mwalimu katika muda wa dakika thelathini ambazo waratibu wa kumbukumbu hii wamempatia. Anasema atakachozungumzia yeye ni kama dibaji tu ya kazi za Mwalimu. 

Anaanza kwa kusema kuwa ukitaka kuzungumzia kazi za Mwalimu ni lazima kichwani kwako uelewe kuwa Mwalimu alikuwa ni mtu mwenye kupenda kubadilika, anasema hadi Mwalimu anafariki katika umri wake mkubwa aliokuwa nao, akili yake bado iliweza kufikiri kileo. Anatoa mfano kuwa wakati kuna watu wengi ndani ya CCM, ambacho kilikuwa ni chama cha Mwalimu hadi mauti yanamkumba, kilikuwa kikipinga kabisa kabisa ujio wa sera ya vyama vingi, Mwalimu hakuona aibu kusimamia kidete ujio wa mabadiliko yale kwani alikwishaona wimbi la mabadiliko yaliyokuwa yakitokea ulimwenguni. Jenerali anasema kuwa, “Usisahau kuwa Mwalimu alikuwa ni kiongozi wa kwanza kufutilia mbali mfumo wa vyama vingi hapa nyumbani lakini muda wake ulipopita hakuona haya kusema kuwa jitayarisheni kwa mabadiliko.” 

Jenerali anasema tuache unafiki kwa kuendelea kuhimizana kumkumbuka Mwalimu kwa maneno na kusahau matendo yake. Anasema ukitaka kujua kuwa tumejaa unafiki basi tazama “watawala” ulionao leo. Jenerali anasema Mwalimu alikuwa ni kiongozi mzuri kwa matendo na si blaablaa, lakini leo hatuna viongozi bali tunao watawala, kitu cha kusikitisha kabisa katika swala zima la uongozi bora. Anasema watawala wetu wanatumia nguvu kubwa sana kuyakandamiza mawazo chanya ambayo yanatishia uwepo wao, anatukumbusha kuhusu mauaji ya Mwembechai (Kumbuka mauaji haya ndio yaliyomnyang’anya Ulimwengu haki ya kuitwa Mtanzania), anatukumbusha pia kuhusu umwagaji wa damu kule Pemba na Unguja. 

Jenerali anazungumzia katiba ya nchi sasa. Anasema, “Niliwahi kumuuliza Mwalimu kuhusu katiba ya nchi yetu ilivyomsaidia katika utendaji wake akanijibu kuwa katiba hii, ambayo tunayo hadi sasa, ilimpa madaraka makubwa kupindukia. Akaniambia kwa katiba hiyohiyo angetaka kuwa dikteta angekuwa, na kweli kwa kiasi fulani alikuwa.” Jenerali anasema kwa kiasi fulani Mwalimu alimudu kuwa dikteta kutokana na nguvu yake ya ushawishi kwa watu, aliweza kusimama mbele ya watu na kuwaambia wasimchague mtu fulani kwa kuwa alikuwa akipingana na siasa zake, na watu walifanya hivyo (Kumbuka sakata la uchaguzi wa mgombea wa CCM kule Dodoma mwaka 1995). Lakini alijaribu sana kutotumia nguvu ya katiba, alitumia nguvu ya ushawishi wake binafsi. 

Tunaambiwa katika utendaji wake, Mwalimu alikataa katakata kuwa kama wenzake kina Mobutu na jirani yake Mzee Kenyatta, wezi wakubwa wa mali ya umma. Anasema Mwalimu angeliweza kabisa kuwaambia kina Edwini Mtei kuwa watoe kiasi fulani cha mamilioni ya fedha na kuzipeleka kwenye akaunti yake binafsi kule Uswizi (kama kweli alikuwa nayo), lakini roho yake katu haikumtuma hivyo, hadi anatoka madarakani kwa hiari. 

Jenerali anagusia swala la kazi za Mwalimu na amani ya Tanzania. Anatukumbusha kuwa wanasiasa wa leo wanacheza na akili zetu, wanatumia neno “amani” kama sera ya kuwatisha watu wasifanye mabadiliko ya kuchagua siasa mbadala kwa kisingizio cha kutoweka kwa amani. Jenerali anasema, “Mwalimu kwa maeneno yake mwenyewe aliwahi kuasa kuwa amani si sera bali ni matokea ya kazi nzuri inayofanywa na siasa safi.” Jenerali anamaliza hoja hii kwa kusema, vita ya kesho inatengenezwa leo na viongozi mafisadi na wala vita ya kesho haitaletwa na mabadiliko ya kisiasa katika nchi hii.

Akizungumzia ufisadi hapa Tanzania, Jenerali anasema, “Ufisadi haukuanza leo. Huko vijijini, ambako mimi nimefanya kazi kwa miaka mingi, vitu hivi vimeanza zamani na ufisadi umeota mizizi zaidi kule, hapa mjini ni rasharasha tu.” Anasema mwalimu aliliona hilo mapema sana, na mara tu baada ya kung’tuka kwake, Mwalimu alilivalia njuga kwa kuanzisha kitu alichokiita “Mradi wa Kubadili Chama”, mradi uliomchukua Mwalimu muda wa miaka miwili kuukamilisha. Mwalimu alichukua jukumu hilo kufuatia mikutano ya kichama aliyokuwa akihudhuria na kuona baadhi ya viongozi walipokuwa wakitoa hotuba zao kiasi kwamba akafikia hatua ya kujiuliza, “Hivi mimi (Nyerere) na huyu anayezungumza hapa, tunatoka chama kimoja?” Usishangae leo unapoambiwa kusaini mkataba hotelini London hakuna shida. Mwalimu alijaribu kung’oa baadhi ya magugu hayo, lakini machache tunayoyaona leo yalikuwa bado kuchipua. 

Naona mratibu wa shunghuli hii anapanda kumwambia Jenerali amemamliza muda wake, anazomewa, watu wanataka Jenerali aendelee kusema nao. Jenerali, hana budi, anamaliza dakika zake thelathini alizopewa kwa kusema, “Ni lazima taifa la leo kujenga upya ujasiri ambao umefifia sana kwa sasa. Ni lazima tujenge ujasiri wa kupambana na utumwa wenye jina jipya. Zitto Kabwe leo amezuiliwa kufika hapa kuadhimisha siku ya muasis wa taifa lake kwa sababu ya ujasiri wake wa kuuliza mambo fulanifulani. Tunasema mabadiliko yanakuja na mafisadi hawana budi kukaa tayari… 

Lazima tujenge upya ujasiri tuliopoteza, na mimi nitaanza kwa kumuuliza waziri wangu wa Fedha, Bi. Zakia Meghji kuhusu bajeti yetu ya mwaka huu kama imeshafika toka Washington. Kutokana na kuuza kwetu ujasiri wetu, tumeuza hata haki yetu ya kujipangia mambo yetu. Nitamuuliza Meghji, bajeti itatumwa lini, maana siku hizi inawezekana kabisa anatumiwa kwa barua pepe, ana-print tu na kwenda kuisoma bungeni. Nasema tujenge ujasiri kama wa Mwalimu. Asanteni”  

Jenerali anashuka jukwaani, anafanyiwa kitu kinaitwa “Stand-up Ovation” yani watu wanasimama na kupiga makofi kwa kama dakika mbili hivi kabla ya kuendelea na maswala mengine.

Picha na Bob Sankofa

Mahala: UDSM

Advertisements

3 Responses to “JENERALI ULIMWENGU NA KAZI ZA MWALIMU”

 1. Asante Sankosa. Taarifa hii kuhusu maadhimisho ya siku ya Mwalimu Nyerere imenipa picha halisi ya kilichotokea na klilichozungumzwa. Umeandika vema, Mungu akubariki.

  Hata vivyo, kuna mambo machache ambayo unahitaji kuyakosoa.

  Kwanza, baadhi ya picha zinaonyesha watu tofauti na wale wanaotajwa kwenye maelezo ya picha. Pili, baadhi ya ‘facts’ haziko sahihi. Kwa mfano, Nyerere hakwenda Uingereza kusoma shahada ya kwanza. Ilikuwa shahada ya uzamili. Vile vile, Ulimwengu hakuvuliwa uraia kwa sababu ya mauaji ya Mwembechai, bali kwa sababu ya mtiririko wa mambo mengi aliyokuwa akikosoa serikali katika maandishi yake, likiwamo suala la ubadhirifu wa Dk. Hassy Kitine. Kwa ubabe wa serikali ya Mkapa, ilikuwa dhambi kuikosoa serikali yake, na hiyo ndiyo njia waliyochagua ya kumshushua anayeikosoa serikai yake.

  Yapo mengine madogo madogo unayohitaji kurekebisha kwa sababu yakibaki hivi ujue yatakuwa hivyo kama historia iliyopotishwa. Naamini usingependa kuandika historia potofu.

  Kijumla umeandika vema. Mengi niliyoyasoma hapa sikuyaona pengine popote. Umenikuna.

 2. haki Blog said

  Mkubwaaa shukrani sana kwa manenoo yenyee
  kuelimisha jamiiii kutoka kwa wakubwa hawaaa..
  nimevutiaa kwa kiasi kikubwa na kazii yako hii
  uliyowakilisha hapa Bob..
  Sasa ombi kwako nifanyie mchakato kama huuu wa mzee
  joseph butiku siku ile pale mlimani…
  Naomba kuwasilisha Ombi
  Admin
  http://www.haki-hakingowi.blogspot.com

 3. kazi nzuri sana na inafurahisha.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: