Kuna wakati fulani Ndesanjo wa www.jikomboe.com aliwahi kuandika kuhusu kasichana kake ka kwanza kabisa, kaliitwa nani tena vile? Stela, bonyeza hapa usome zaidi.
Basi hata mimi pia nimewahi kuwa na “Stela” wangu pia, Wangui wa Kimari, mtoto toka Kenya huyu. Nilikutana naye wapi tena vile? Ahh, ni pale chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka ule wa 2004/2005. Wangui alikuwa akisoma Carlton University, Canada na alikuwa amekuja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kitu kinaitwa Exchange Program (Kiswahili chake baadae).
Nakumbuka alinikaribisha chumbani kwake jioni moja, pale hall 3, kwa chai ya jioni. Nilikwenda, tulikuwa wawili tu chumbani lakini sikuweza kumwambia chochote. Akanitengenezeza kikombe cha chai, nikanywa.
Nakumbuka pia kuwa muda mwingi yeye ndiye alikuwa akiongea zaidi. Mimi nilikuwa nasikiliza zaidi. Aliniuliza napenda mziki wa aina gani, nikamwambia Afrika Magharibi, na muziki mwingine wowote wa kimapinduzi. Basi alikuwa na CD ya Michael Frant (Mcheki huyu jamaa kwenye Google, ni mtu matata sana), akaweka. Hii CD alikuja kunipa kama zawadi wakati alipokuwa akiondoka kurudi Canada.
Basi tukaendelea kunywa chai na kusikiliza ‘madongo’ ya Frant. Nilikuwa na nywele za msokoto (dredlocks) kipindi kile, akazishika na kuniambia kuwa alizipenda. Moyo ukanilipuka. Yeye pia alikuwa na nywele msokoto (Anazo hadi leo), nikamwambia nazipenda za kwake pia. Sikuweza kuendelea kuongea zaidi.
Kabla sijakaa sawasawa mwenzake ambaye walikuwa wakikaa chumba kimoja akarudi toka darasani, siku ile ikawa ndo imekufa tena. Shabaaaash, nilimlaani sana rafiki yule, kimoyomoyo lakini, kwani kaujasiri ka kusema jambo kalishaanza kuniingia. Read the rest of this entry »