MWENYEMACHO DOT COM

Yanapojiri Nilipo na Wewe Upo

PROFESA ISSA SHIVJI ALIVYOMKUMBUKA MWALIMU

Posted by Bob Sankofa on October 15, 2007

062.JPG

Tumerudi kwenye ngwe ya pili ya kumjadili Mwalimu baada ya mapumziko mafupi. Wa kwanza anayepewa nafasi ya kumzungumzia Mwalimu kwa sasa ni mhadhiri wa Sheria wa siku nyingi, Profesa Issa Shivji. Shivji pia ni mmoja wa Wajamaa wachache waliosalia wanaoishi katika jamii ya kibepari. Kwa wale wenye tatizo na Richa Adhia, mrembo wa Tanzania 2007, nadhani watakuwa na tatizo pia na uhalali wa u-Tanzania wa mhadhiri huyu. Haituhushu kwa sasa tuendelee. 

Katika kumjadili Mwalimu, Shivji anaanza kwa kusema, “Huu si tu mwaka wa 8 toka Mwalimu kufariki bali pia ni mwaka wa 40 tangu kuzaliwa kwa Azimio la Arusha. Mbona wote tumesahau basi kukumbuka kuuawa pia kwa Azimio? Hata Taasisi ya Mwalimu pia imesahau hilo, ingekumbuka ingetutahadharisha katika kutengezeza kauli mbiu ya kumkumbuka Mwalimu na marehemu mwanae, Azimio la Arusha.” 

Profesa Shivji anasema kusahau huku kulikumbuka Azimio kumewafanya viongozi wetu pamoja na sisi wenyewe kusahau kile anachoita “haki ya Mungu” na kuithamini “haki ya Mzungu”. Shivji anamaanisha kuwa Watanzania tumeuza utu wetu kwa kukimbilia pesa za mzungu. Mwenye pesa ndie mwenye kusikilizwa siku hizi. Shivji anauliza ingekuwa vipi iwapo hali tuliyo nayo ingeanzia enzi za Mwalimu? Shivji katika kujadili kwake pia anasema, amekuwa akisikia watu wakilalamika sana kuwa Tanzania hatuna dira tena, tofauti na ilivyokuwa enzi za Mwalimu.

Anauliza, “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania sio dira?” Halfu hapohapo anajijibu mwenyewe, “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania sio dira(vision) bali ni mradi(project)” Watu wanacheka. 

Shivji anasema tofauti na Azimio la Arusha ambayo ilikuwa dira kwa wananchi wote kwa sababu azimio lilitokana na watu wenyewe, Maisha Bora kwa Kila Mtanzania ni mradi wa mtu fulani na tayari wenye akili wameshajua mradi ule utamfaidisha nani kwani wanaofaidika tayari wameshaanza kuonekana. Watu wanabaki wamepigwa na butwaa kwani hapa nilipokaa nimekaa karibu kabisa na Waziri wa Ardhi, Mh. John Pombe Magufuli ambaye anatabasamutabasamu tu. 

Shivji alipewa dakika kumi na tano tu na anaambiwa zimebaki mbili, anamaliza kwa kusema, “Ndani ya miaka 15 Tanzania imezama na kujichimbia katika hatari kubwa ya matabaka. Anasema sasa hivi tunaona dhahiri uwepo wa Walala heri (wenye maisha safi hawa) na Walala Hoi (masikini wa kutupa)” Ah! Amesahau, eti hapo katikati kuna Walala Hai (watu kama yeye) ambao wanaota kuwa siku moja watapanda kuwa Walala Heri lakini kila kukicha wanajiona wakizidi kuelekea kwenye tabaka la Walala Hoi. 

Amemaliza na ameshatoweka tayari. Watu wamefurahishwa naye mno.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: