MWENYEMACHO DOT COM

Yanapojiri Nilipo na Wewe Upo

TUNAKUINUA TUKITAKA, TUNAKUDONDOSHA TUKITAKA!

Posted by Bob Sankofa on August 31, 2007

oj-simpson.jpg

Duka la vitabu la Barnes & Noble Inc. pale Marekani, baada ya kukataa katukatu kuuza kitabu cha O. J. Simpson hatimaye wamebadili msimamo wao na kulamba matapishi yao.

Unamkumbuka OJ, ni yule mchezaji wa mpira wa miguu (japo muda mwingi hutumia mikono) wa Kimarekani, ambaye mwaka 1994 alishutumiwa kumuua mkewe pamoja na mpenzi wa mkewe ambao eti aliwabamba live kwenye gari lake la kifahari “wakiiba” penzi. Kesi yake ilikuwa tata sana, nakumbuka baba yangu alikuwa ni mtu wa mwisho kila siku kulala akiifuatilia kupitia CNN, na siku OJ aliposhinda alifurahi utadhani ni Mmarekani. Nafikiri watu weusi karibu wote duniani walifurahi kwa sababu toka mwanzo kesi ilikuwa ikiendeshwa kwa misingi ya kibaguzi na hivyo kujenga kambi mbili, za watu weusi (waliokuwa upande wa OJ) na watu weupe (waliokuwa upande wa mke wa OJ na hawara yake ambao wote ni wazungu)

OJ alishinda kesi ile kwa ushahidi kabambe na hoja nzito nzito ambazo upande wa mashitaka ulishindwa kuhimili, lakini bado rufaa ilikatwa na familia za wahanga (Marehemu) na wakafanikiwa kuhakikisha kuwa OJ anafilisiwa, sikuwahi kuelewa na sitakaa nielewe, ni kwa nini ilikuwa hivi. Labda atokee mwanasheria wa kutusaidia hapa bloguni kuwa ni kwa nini ilikuwa vile.

Sasa wale jamaa wa Barnes & Noble Inc. walisema wazi kwamba hawatakuwa tayari kuuza kitabu kile kwani hapakuwa na wateja wa kutosha wa kununua kitabu kile, Duka hilo lilisema hayo kwa shirika kubwa la habari liitwalo Associated Press. Lakini Alhamisi ya jana ikabadili msimamo na kusema itakiweka kitabu hicho sokoni. Hii inaonekana wazi kabisa kuwa bado wazungu wana hasira na OJ na wana mpango kabambe wa kuhakikisha hafanikiwi katika kila biashara anayoanzisha hadi ageuke “Matonya” kabisa, lakini katika ulimwengu wa mtandao wateja wamewaumbua kuwa madai yao hayakuwa ya kweli.

Tangu tarehe 21/8 duka hilo lilisema wazi halitakuwa tayari kuuza kitabu hicho dukani bali lilikuwa tayari kuuza kitabu hicho mtandaoni. Msemaji mkuu wa duka hilo bibi Mary Ellen Keating alisema, “Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu oda za wateja wetu, na wengi wao wameonyesha kuwa watahitaji kukinunu na kukisoma kitabu hiki toka hapa dukani kwetu. Katu “hatutakitangaza” kitabu hiki lakini tutakiweka hapa dukani kwa sababu wateja wetu wanakiulizia.”

Kwa siku kadhaa kitabu hicho cha bwana OJ kimekuwa katika orodha ya vitabu 100 vinavyosubiriwa kwa hamu katika mtandao wa Barnes & Noble.com. Kitabu chenyewe kinakwenda kwa jina la “If I Did It”, na pia kipo katika vitabu mia moja vinavyongojewa kwa hamu pale Amazon.com.

Kitabu hicho kimeandikwa kinadharia kikielezea jinsi ambavyo OJ angewaua wanaodaiwa kuwa wahanga wake, yani mkewe, Nicole Brown Simpson pamoja na “mwizi” wake Ronald Goldman, iwapo ni kweli aliwaua yeye. Kitabu kilikuwa kitoke Novemba, mwaka jana lakini mchapishaji, HarperCollins, alisitisha zoezi hilo kwa kile alichodai kuwa ulimwengu, akimaanisha wazungu wenye mtazamo hasi, ungeandamana kupinga mauzo ya kitabu hicho.

Sasa cha kushangaza ni kwamba japo kitabu ni cha OJ na kinamhusu OJ, jaji wa masuala ya kesi za kufilisi watu ameamua kwamba faida yote itakayotokana na kitabu hicho itachukuliwa na familia ya bwana Goldman ambaye anadaiwa kuuawa na OJ baada ya OJ kustuka kwamba jamaa alikuwa anamwibia mkewe. Mahakama imeamua hivyo ili eti fedha hizo zitumiwe na familia ya bwana Goldman kuendeleza uchunguzi wa kifo chake, uchunguzi ambao hadi sasa unagharimu dola za Kimarekani 38 milioni. Na wakati huohuo familia hiyo inachukulia kitabu hicho kama ni kukiri kwa OJ kufanya mauaji hayo.

OJ amekuwa akishikilia kuwa hakufanya mauaji hayo ya mwaka 1994, na mahakama ilithibitisha hivyo katika kesi yake ambayo iliigawa Marekani na dunia katika matabaka ya watu weusi na watu weupe kwa muda. OJ ambaye kwa sasa anaishi na watoto wake karibu na jiji la Los Angeles, amekikana kitabu hicho hivi karibuni kwa madai kwamba mwandishi wake mkuu, bwana Pablo Fenjves, ameandika mambo mengi ya ziada amabyo hayana ukweli. Pablo amekanusha kwa kusema alimshirikisha OJ katika ngazi zote.

Tunaishi katika ulimwengu wa ajabu kabisa, ulimwengu wa kutoana kafara, sisi ndi Wamarekani, tunao uwezo mkubwa kabisa wa kukuinua na kukufanya maarufu tukitaka na tunao uwezo mkubwa wa kukudondosha na kubaki ombaomba tukitaka. Upo?

Hadi wakati mwingine,

UHURU!

Habari kwa msaada wa tovuti kadhaa za habari

Picha kwa msaada wa Google Search

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: