MWENYEMACHO DOT COM

Yanapojiri Nilipo na Wewe Upo

MAITI YA CHE – MOJA YA PICHA 13 ZILIZOSIMAMISHA ULIMWENGU

Posted by Bob Sankofa on August 23, 2007

che-corpse-freddy-alborta.jpg 

“Mwendawazimu”, “mzuka”, “balaa”, “shujaa”, “mkombozi”. Hayo ni baadhi ya majina ambayo yule mwanaharakati na mwanamapinduzi Ernesto “Che” Guevara alipata kubandikwa. Mwanazuoni Jean-Paul Sartre alipata kusema, “Che ni mwanadamu mkamilifu aliyepata kuishi wakati wetu”. Unaweza usikubaliane katukatu na mwanazuoni huyu lakini katu hutoweza kubisha ya kuwa Ernesto ndiye Baba Mtakatifu wa Kimapinduzi. Nasikia hata yule mbunge wenu waliyemtimua kule Dodoma anamhusudu sana huyu bwana. Sina hakika na hilo, mimi pia nimesikia tu. Sina hakika, walahi tena, sina hakika kabisa. Mimi nakubaliana kabisa na mwanazuoni huyo hapo juu kwa sababu heshima ya Che imejengeka zaidi baada ya kufa kwake kuliko hata wakati alipokuwa akiishi.

Che alipenda kutetea wanyonge, masikini na waliokandamizwa. Alitembeza libenenge la ajabu kule Kuba. Unayo habari kwamba aliwahi kushusha libenenge pale Kongo? Aliamua kuendeleza libenenge hadi kule nchini Bolivia ambako alitengeneza timu na watu maiskini na waliokuwa wakinyonywa na utawala fedhuli wa kijeshi (Jeshi lile lilikuwa likifunzwa na kufadhiliwa na serikali ya Marikani na C.I.A). Kwa bahati iliyo mbaya, libenenge la Bolivia halikukaa vyema na Che akakamatwa na kuuawa mwaka 1967.

Lakini kabla ya kuutupa mwili wake katika kaburi lisilojulikana, wauaji wake wakauzunguka mwili wa mwanamapinduzi Che ili kupiga naye picha huku wakimfanyia dhihaka. Walitaka kuuthibitishia ulimwengu wa wanamapinduzi kwamba Che amefika tamati na hivyo hata libenenge limefikia tamati pia. Wakiwa na hofu kwamba watu wasingeamini kwamba Che amekufa kweli, wauaji wake walikata mikono yake na kuihifadhi kwa dawa inayoitwa “formaldehyde” ili isioze na iwe udhibitisho. Je kwa kufanya hivi walikuwa wakimtukuza au wakimuangamiza?

Ukweli ni kwamba, kwa kumuua mwanamapinduzi huyu, mabwana wakubwa wa Bolivia walikuwa wakimtukuza bila ya ufahamu wao. Mara picha hii ilipoingia mitaani watu wengi waliifananisha na ule mchoro maarufu wa Nabii Yesu Kristo alipokuwa akishushwa msalabani. Ukiangalia huyo askari jeshi wa upande wa kulia anaonyesha kwa kidole chake mahala ambapo risasi ilipigwa na kumuua Che, kidonda kile wanamapinduzi wamekifananisha na kidonda cha mwisho cha Yesu kilichotokana na kuchomwa mkuki na mabwana wakubwa wa Kirumi. 

Ukiangalia kwa makini utaona kuwa Che alikufa akitabasamu. Wanamapinduzi wameichukulia ishara hii kama alama ya msamaha wa Che kwa wauaji wake kwa kuwa hawakujua walilokuwa wakifanya.

Mabwana wakubwa wa Bolivia walidhani picha ile ilikuwa ndio tamati ya Che na mawazo yake. Unadhani kilifuata nini baada ya hapo? Ulizaliwa msemo maarufu unaodumu hadi leo, “Che lives!”. Shukrani kwa mwabwana wakubwa wa Bolivia kwa kupiga picha hii kwani imechangia kwa kiasi kikubwa sana kuendelea kuishi kwa Che na mawazo yake hata leo.

Chukua kisa hiki na ukitumie kama kipimo cha vuguvugu la kisiasa nchini kwako leo. Unaona nini?

Hadi wakati mwingine,

UHURU!

Picha kwa msaada wa Google Search Engine

Modeli: Che na Mabwana wakubwa wa Bolivia

Mahali: Bolivia

Advertisements

4 Responses to “MAITI YA CHE – MOJA YA PICHA 13 ZILIZOSIMAMISHA ULIMWENGU”

  1. Bob,
    Sikuwahi kuiona picha hii kabla.Asante kwa kuiweka hapa.Hivi karibuni niliandika jambo pale kwenye Harakati ambapo niliweka pia kiungo chenye documentary ya maisha ya huyu bwana.Ninahusudu sana uanamapinduzi aliokuwa nao Che.

  2. Nilipata mzuka wa kuandika post hii baada yay kutembelea pale kwako na kufuata viungio ulivyoweka pale. Asante kwa kupita hapa na kusabahi.

  3. luihamu said

    Safi Bob,Che ni mwanamapinduzi wa kweli.

  4. mnyikungu said

    mapinduzi ya kweli huja na fikra pamoja na ujasili wa kweli.Che ni mfano wa kuigwa na wanaharakati na wapenda haki na usawa pote duniani.kumuenzi che kwa WAAFRIKA NI KUZIPIGANIA RASILIMALI ZETU ZILIZOPO ILI ZITUNUFAISHE WAAFRIKA WENYEWE.KUONGEZA UJASILI KATIKA KUPAMBANA NA SELIKALI DHALIMU ZINAZOTAWALIWA NA MAFISADI PAMOJA NA VIBARAKA WA MAGHARIBI.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: