MWENYEMACHO DOT COM

Yanapojiri Nilipo na Wewe Upo

JIFUNZE FOTOGRAFIA KWA KUTUMIA MITANDAO YA PICHA

Posted by Bob Sankofa on August 15, 2007

ethiopian-coffee.jpg 

Zamani ukitaka kujifunza kuwa mwanafotografia ilikuwa ni lazima uende chuo cha mafunzo na ulipe ada kubwa, kweli si kweli? Yuko mwalimu mmoja wa fotografia anaitwa Ibarionex R. Parello, Parello amewahi kuandika insha inaitwa “Learning from Sharing Photos Online”, katika insha ile anasema zamani hakuwahi kuwa na marafiki wengi wa kumhamasisha kupiga picha. Mahala pekee ambapo aliweza kupata hamasa ilikuwa ni ama kwenye jumba la maonyesho ya picha au kwenye majarida aliyokuwa akinunua kila mwezi.  

Anaendelea kusema kuwa muda haukumruhusu kila mara kutembelea jumba la kuhifadhia picha na hakuwa na pesa ya kutosha kuagiza jarida la picha kila mwezi pia. Mtandao wa intaneti umebadili yote haya, tena kwa kasi kubwa, anasema Parello. Tovuti za picha pamoja na mitandao mingine iliyoanzishwa, kama vile www.flickr.com au www.utata.org, ambayo yote miwili mimi ni mwanachama, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kwa wapiga picha wa kulipwa na wasio wa kulipwa kuweza kuonyesha kazi zao sio tu kwa watu walio karibu nao bali ulimwenguni kote. 

Kwa mtu kama mimi ambaye fotografia si tu chanzo cha kutengeneza fedha bali pia starehe, mitandao hii imekuwa ni chachu kubwa ya kunipatia mawazo mapya ya picha gani nipige katika siku inayofuata. Kuna jambo moja nimegundua kwa kipindi kifupi tangu nimekuwa mwanachama wa mitandao hii miwili. Jambo hilo ni kuwa wapiga picha ambao wanaifanya kazi ya kupiga picha kama kitu cha kujifurahisha na si kutengeneza pesa, kazi zao huwa ni bora zaidi kuliko zile unazoweza kuziona kwenye magazeti kama vile TIMES MAGAZINE. Ukiziona picha zile huwezi kuamini kuwa zimepigwa kwa kutumia kamera ambazo hazizidi hata dola za Kimarekani 150. 

Lakini kinachofurahisha zaidi kwenye mitandao hii ya picha ni kuwa unakuwa na uwezo wa kuwasiliana na wapiga picha wa kazi zile moja kwa moja kwa kutumia barua pepe, na ukawauliza chochote kuhusu kazi zao au kama unalo tatizo katika upigaji picha wako wanakusaidia ndani ya muda mfupi sana. Mimi ninao marafiki wapiga picha wanaokaribia 400 hivi. Wametapakaa ulimwenguni kote, ni wa makabila, umri na rangi mbalimbali bali tunaunganishwa na kitu kimoja, sisi ni wapiga picha. 

Ukiingi mtandaoni huishii kuwa mtazamaji tu, unakuwa mchangiaji, ukitembelea www.flickr.com/photos/mwenyemacho utaweza kujionea picha zangu ambazo ninazirusha humo kila siku iendayo kwa Mungu. Nafurahi zaidi pale marafiki zangu, wapiga picha wanapotoa maoni yao juu ya picha zangu, yani wanakuwa ni chahu kubwa sana kwa maoni yao. Maoni yale yanakupa hamasa ya kuchukua kamera yako kila unapokwenda ili kuweza kuweka picha zaidi katika ukurasa wako. Maoni yale yanakufungua ubongo wako zaidi, maoni yanakufanya uishi na kufikiria nje ya boksi. 

Tafadhali tembelea mitandao hiyo niliyoizungumzia hapo juu na ujifunze mengi katika fotografia. Fotografia si kazi ya mtu fulani tu, hii ni kazi yetu sote, mimi, wewe na yule.  Kanunue au kaazime kamera kwa rafiki na ujiwekee lengo la kupiga picha mbili kwa wiki na kuzirusha kwenye blogu. Picha mbili mara wiki nne utakuwa na picha nane. Picha nane mara miezi kumi na mbili utakuwa na picha 96, je hiyo si tiketi kabisa ya kukufanya wewe kujiita mpiga picha?  Zitume picha zako kwenye mitandao ya picha, acha marafiki watoe maoni na ama kwa hakika kabla ya kufumba na kufumbua utajikuta umekuwa mwanafotografia. 

Hadi wakati mwingine,

UHURU!

Picha na: Bob Sankofa

Model: Wangui wa Kimari

Mahala: Addis in Dar Restaurant

Advertisements

5 Responses to “JIFUNZE FOTOGRAFIA KWA KUTUMIA MITANDAO YA PICHA”

 1. ndesanjo said

  Habari kama hizi nazipenda sana maana zinatuonyesha nji na kuonyesha jinsi gani tunavyoishi au kuingia kwenye zama za kuunganishwa na kuwezeshwa.

  Picha zako unaweza kufikiria kama ungependa kuzitoa kwenye leseni ya Creative Commons (copyleft badala ya copyright). Fikiria hilo jambo, kuna faida zake na pia hili ni jambo linaloendana na itikadi fulani fulani ambazo najua unazo.

 2. luihamu said

  Bob safi sana.

 3. Bob,
  Mimi ni mpenzi sana wa sanaa ya picha.Takribani asilimia 98% ya picha unazoziona kwenye blogs zangu huwa nimezipiga mwenyewe.Kuna watu wameshawahi kuniambia kwamba ninalo “jicho la picha”.Ajabu sijawahi kuiangalia mitandao uliyoitaja kwa jinsi ulivyonifungulia hivi leo.Nadhani sasa umenitia hamasa mpya.Nitafungua nami ukurusa wangu.Asante

 4. Ni kweli Ndesanjo kwa yale usemayo, na nimeshayafanyia kazi mawazo yako.

  Asante Luihamu.

  Kaka Jeff, nafurahi kwamba angalau nitakuwa na Mtanzania mwingine ambaye tutashirikiana mawazo kwenye mitandao ile. Kaka Watanzania hawataki kabisa kushiriki kwenye haya mambo, sina maelezo ya kina ni kwa nini tuko hivi, ila najua jambo moja ni dhahiri, Ulimwengu tulionao ni ulimwengu wa teknolojia na haumngoji mtu, hivyo tusiposhiriki katika mabadiliko haya tutaachwa tena nyuma kama ilivyokuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita. Nashukuru kwa kutembelea hapa na kuyafanyia kazi niliyoandika.

  Niliwahi kutaka kuuliza ni nani anayefanya picha zako, hatimaye umenijibu kabla. Ni kweli kaka unalo jicho hasa, na ukweli ni kuwa nadhani siku hizi kila mtu ana jicho la picha, KILA MTU ANAWEZA KUPIGA PICHA!

  Hadi wakati mwingine UHURU!

 5. ndesanjo said

  Jeff:
  Tulishawahi kuongelea hili suala la picha huko nyuma ukanielekeza kwa baadhi ya watu ambao umeona kuwa wana macho ya picha. Tukaongelea jinsi ambavyo kupiga picha inaweza kuwa ni aina fulani ya sanaa. Tena nakumbuka uliwahi kusema umeanza kutumia sijui ni photoshop au nini, ila kuna zana fulani ya kuhariri picha ulikuwa unacheza nayo.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: