MWENYEMACHO DOT COM

Yanapojiri Nilipo na Wewe Upo

BINTI WA KIMARI

Posted by Bob Sankofa on July 27, 2007

princess-wangui.jpgKuna wakati fulani Ndesanjo wa www.jikomboe.com aliwahi kuandika kuhusu kasichana kake ka kwanza kabisa, kaliitwa nani tena vile? Stela, bonyeza hapa usome zaidi.

Basi hata mimi pia nimewahi kuwa na “Stela” wangu pia, Wangui wa Kimari, mtoto toka Kenya huyu. Nilikutana naye wapi tena vile? Ahh, ni pale chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka ule wa 2004/2005. Wangui alikuwa akisoma Carlton University, Canada na alikuwa amekuja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kitu kinaitwa Exchange Program (Kiswahili chake baadae).

Nakumbuka alinikaribisha chumbani kwake jioni moja, pale hall 3, kwa chai ya jioni. Nilikwenda, tulikuwa wawili tu chumbani lakini sikuweza kumwambia chochote. Akanitengenezeza kikombe cha chai, nikanywa.

Nakumbuka pia kuwa muda mwingi yeye ndiye alikuwa akiongea zaidi. Mimi nilikuwa nasikiliza zaidi. Aliniuliza napenda mziki wa aina gani, nikamwambia Afrika Magharibi, na muziki mwingine wowote wa kimapinduzi. Basi alikuwa na CD ya Michael Frant (Mcheki huyu jamaa kwenye Google, ni mtu matata sana), akaweka. Hii CD alikuja kunipa kama zawadi wakati alipokuwa akiondoka kurudi Canada.

Basi tukaendelea kunywa chai na kusikiliza ‘madongo’ ya Frant. Nilikuwa na nywele za msokoto (dredlocks) kipindi kile, akazishika na kuniambia kuwa alizipenda. Moyo ukanilipuka. Yeye pia alikuwa na nywele msokoto (Anazo hadi leo), nikamwambia nazipenda za kwake pia. Sikuweza kuendelea kuongea zaidi.

Kabla sijakaa sawasawa mwenzake ambaye walikuwa wakikaa chumba kimoja akarudi toka darasani, siku ile ikawa ndo imekufa tena. Shabaaaash, nilimlaani sana rafiki yule, kimoyomoyo lakini, kwani kaujasiri ka kusema jambo kalishaanza kuniingia.

Wangui, mrembo wa roho yangu, nakumbuka alikuwa akipenda sana kusoma vitabu vya kimapinduzi, mimi pia. Yeye alimpenda sana mwandishi aliyekuwa akiitwa James Baldwin, mimi nikimpenda zaidi Cheikh Anti Diop na zaidi Shaaban Robert. Kwa hiyo muda mwingi ilikuwa tukikutana tunaongea kidogo sana kutuhusu mambo yetu wenyewe na kwa muda mrefu ni kujadili kuhusu fikira za kimapinduzi na vitabu tulivyokwishasoma au ambavyo tulikuwa tunasoma kwa wakati huo. Nikirudi chumbani siishi kujilaumu kwa nini sikumwabia kuwa nampenda, halafu najiwekea nadhiri kuwa nikikutana naye tena ni lazima nitamwambia ukweli wa mambo. Siku ikifika spidi ni ileile ya kujadili vitabu vya Baldwin na Diop na wengineo kama hao.

Muda haugandi bwana, mwaka ukaisha na binti Kimari akatakiwa kurejesha majeshi Carlton, kumalizia shahada yake ya mambo ya kale. Sikumbuki kama niliwahi kutoa machozi kwa kumuaga mtu ila nakumbuka kufanya hivyo punde tu Wangui aliponipa kisogo, na mimi sikuwa nimemweleza chochote. Hakuniona nikilia lakini.

Nakumbuka, baada ya siku kadhaa nilimwandikia ujumbe mrefu sana wa barua pepe kumweleza yaliyokuwa yakinisibu, niliandika kwa mtindo wa kishairi. Mungu akipenda nitalirusha shairi lile hupa siku moja.

Unadhani alinijibu nini? Alijibu, pia kwa barua pepe, kwa ufupi sana (Mistari kama mitano hivi), kwamba nilikuwa nimechelewa kidogo. Ati ningemwambia mapema labda angenifikiria :-). Lakini kwa sasa uhusiano wetu kwa kaisi kikubwa ulikuwa umeshajikita katika ukaka na udada. Likanishuka “pwaaaaaaaa!”. Ila mwishoni alisema kuwa alinipenda pia kwa kuwa wote tulikuwa tuna mawazo mamoja. Wote tulipenda kusoma vitabu.

Mwaka ukapita, tuakamaliza shahada zetu. Kwa muda mrefu sana baada ya kutoka shuleni hatukuwasiliana na Wangui, nilikuwa naona aibu kubwa kumwandikia. Ndio je, si nilikuwa nimeharibu sasa? 🙂

Siku moja nafungua sanduku langu la barua pepe nikakuta barua pepe toka kwa Wangui lakini iliandikwa kwa Kireno. Kumbe kipindi chote hicho Wangui alikuwa amehamia Brazil na alishajifunza Kireno kwa kiasi kikubwa. Wangui akanimbia imekuwa kitambo sana hatujawasiliana lakini alikuwa na imani kuwa naendelea vizuri. Aliitafsiri ile barua kwa kiswahili kwa chini.

Alikuwa amefurahi kwani alikuwa anarejea nyumbani, Kenya, baada ya kuwa nje kwa muda mrefu. Aliniahidi kuja Dar es Salaam kuniona, akipata japo nafasi. Nikafurahi kwamba angalau nitamwona barafu wa moyo wangu kwa mara nyingine. Haikuwa kwa haraka hivyo, ikapita miezi mingine saba, hadi juma lilopita ndio Wangui akaingia tena Dar.

Sikuamini kuwa nilikuwa namwona Wangui mbele yangu, tukakumbatiana kwa muda wa dakika mbili nzima. Ni kitambo sana. Tukaongea na kunywa mvinyo. Alisikitika kuwa nilikata nywele msokoto zangu. Mimi nilishangaa kwa jinsi nywele msokoto zake zilivyokuwa ndefu kiasi kile, nilizipenda zaidi.

Wangui alitaka kufikia hotelini nikamwambia hapana, akaribie nyumbani kwetu. Akakubali. Nikafurahi. Wangui hakuwa amebadilika sana toka mara ya mwisho nilipomuona. Ila alizidi kuwa mzuri. Alikuwa akiongea zaidi, Kiswahili chake cha kiNairobi, mashalaaaah! Mimi kama kawaida, nasikiliza zaidi.

Tuliongea mengi katika siku zake tatu alizokaa hapa Dar. Alifurahi kusikia kuwa nina blogu ya kiswahili na kuwa ninafanya fotografia pia. Akaniambia yuko mbioni kurudi Brazil wiki mbili zijazo. Akaniambia kuwa alikuwa anakwenda kufanya Stashahada ya mambo ya kale. Nikafurahi kwa hatua anayopiga. Akaniuliza kuhusu mustakabali wangu, nikamwambia kuwa nguvu zangu zimeelekezwa kwenye fotografia sasa. Nataka kusoma zaidi kuhusu fotografia. Akafurahi.

Akaenda mbele zaidi na kuniuliza, “Sankofa, how is your love life?”. Nilijibu nini unadhani? Mtu akiniuliza swali ambalo hunitatiza kidogo huwa nabadili lugha, nadhani huwa inapunguza makali ya mjadala. Ni imani yangu lakini. Nikamjibu, “I’ve been seeing girls but nithing is working out so far”. Halafu fasta nikabadili gia, nikamwita muhudumu aniongeze mvinyo. Nilifanikiwa kubadili mad kwa gia ile. 🙂

Siku iliyofuta, Wangui alitaka kutembelea Bagamoyo, kuona marafiki pale pamoja na mambo ya kale. Tukaendea, na nikamwomba kumpiga picha nyingi kwa kadri ya uwezo wangu, tembelea www.flickr.com/photos/mwenyemacho, utaziona. Alinikubalia. Picha hii uionayo hapa niliipiga Jumanne ya juma hili. Ahh Wangui wa Kimari, wacha nisononeke mie, u mrembo bibie, hakuna mwanaume ambaye hatasononeka juu yako.

Basi mchana wa jumanne ile tukarejea zetu Dar na jioni tukaelekea kwenye mgahawa mmoja wa kiafrika unaitwa “Addis in Dar”. Tulikunywa mvinyo wa asali pale, na chakula cha Kiethiopia. Safi sana mlo ule. Basi nafikiri nishai ilikuwa imenitoka kidogo, nikapata kaujasiri ka kuibua kale kamjadala ka mapenzi nilikokaanzishaga miaka ile kwenye barua pepe. Unakumbuka kuwa kamjadala kale Wangui alikazima kwa haraka sana kipindi kile?

Basi nikamtamkia mbele ya macho na msikio yake kuwa nampenda bado, tena nampenda kwelikweli. Wangui akaniangalia kwa huruma na kuniomba msamaha iwapo ataiumiza roho yangu. Wangui aliniambai kuwa sababu moja wapo ya kutafuta shule kule Brazil ni kwamba alipata mpenzi kule na shule ndio namna pekee ambayo ingemwezesha kuwa karibu na mpenzi yule.

Moyo ukalipuka pwaaaaaaaaaaaa! Nikajikuta natoa tu tabasamu mgando na kujidai nimeelewa. Wangui akaniomba sana nisijisikie vibaya eti. Nikamwitikia, “Positive”. Ningeachaje kujisikia vibaya?

Akaniomba nimtembelee Brazil kwa haraka iwezekanavyo. Nikamkubalia. Nikaweka nadhiri kuwa nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote ili niweze kununua tiketi ya ndege na Mungu akipenda nitakwenda kumuona Wangui wangu mapema mwakani. Nakwenda kweli ujue?

Sikumbuki sawasawa kwa nini niliweka nadhiri ile kwa haraka namna ile. Unajua nadhiri ikiwekwa hubakia nadhiri hadi itimizwe hivyo lazima niitimize.

Safari ile labda itakuwa ni ya kwenda kumsalimu Wangui na pia kupiga picha maeneo ya Brazil. Wangui ananiambia kila kona ya mitaa ya Salvador utakuta watu wakipiga muziki na kucheza kapoera. Nafikiri nitarudi na picha lukuki za utamaduni wa watu wa Brazil.

Huyu ni Wangui, mrembo niliyempenda kwa moyo, akili na roho yote lakini kila wakati nimechelewa kidogo.

Wangui ameondoka jana kuelekea Kenya kujiandaa kurudi Brazil. Ameniachia zawadi ya kitabu kinaitwa Dogrun, nimempa zawadi ya kitabu pia kinaitwa Dancers on the Shore. Tunapendana japo muda umetuzidi maarifa. Bongo zetu na mioyo yetu imeshabihiana tangu mwanzo lakini miili yetu i dhaifu. Itabaki hivyo, sijui kwa kitambo gani.

Huyu ndiye “Stela” wangu, Wangui wa Kimari. Ndesanjo na Chediel mpo hapo? Kwa picha zaidi tafadhalini tembeleeni www.flickr.com/photos/mwenyemacho

Hadi wakati mwingine,

UHURU!

16 Responses to “BINTI WA KIMARI”

  1. luihamu said

    Mzee,nimesoma na kusoma na kusoma kama mara tatu vilenami pia nitarusha stela wangu karibuni,BOB umenikumbusha mbali sana,nami pia nilikuwa na stella kwa jina la Beatrice sasahivi yuko Nerthalands lakini yeye hakuwa na nywele za msokoto mimi wakati huo nilikuwa na nywele za msokoto na imani kali ya RASTAFARIANS.Ngoja niishie hapo kwa leo.

    Sasa Bob,inamaana baada ya kukata dreadlocks umeacha kusoma vitabu na imani yako?vitabu vya kimapinduzi?

    Bob karibu Rastafarians.

  2. luihamu said

    Bob,naomba ruhusa yako nitumie picha ya Stella katika blogu ya Rastafarians,kuna picha moja kapiga Bagamoyo kashika chombo kinachotoa moshi.Bob natumai utaniruhusu kutumia picha hiyo katika topic moja nayo andaa ya IMANI YA RASTAFARIANS NA BABYLON WORLD.

  3. ndesanjo said

    Da! Sankofa kisa cha Stela wako sio tu kitamu na cha huzuni ila pia umekiandika kwa ufundi mkubwa sana. Nilipomaliza kusoma nilijishtukia kuwa nilikuwa wala sijakaa vizuri kwenye kiti. Ilikuwa karibu nianguke bila kujua. Nadhani visa hivi vina utamu wake na vinatukumbusha mengi ya nyuma na kutoa picha fulani juu yetu. Sio vibaya wengine nao wakatupa visa vya “Stela” wao. Najua Chedieli na Luihamu wapo. Nataka kuwasikia Tunga, Jeff, Simon, n.k.

    Nimetembelea pale Flickr. Unatumia mistari mizuri sana kuelezea picha zako. Na picha za dada yetu…da! Kwanini tusiende wote Brazili?

  4. Luihamu nasubiri kwa hamu kisa cha “Stela” wako. Tafadhali kuwa huru kutumia picha ile, usisahau kueleza ilikotoka na tafadhali usiitumie kwa dhumuni la kibiashara.

    Kaka Ndesanjo asante sana kwa kutembelea flickr, pia asante sana kwa kunipa airtime kwenye blogu yako. Karibu kwa safari ya Brazil kaka, mwezi wa nne mwakani. Tuombe uzima.

  5. Duh!

  6. luihamu said

    Asante Bob,nami nahaidi kutoitumia picha ya Princess katika biashara yoyote ile.Asante Bob.Jah Bless.

  7. Daah! kazi kweli kweli.Pole sana Bob

  8. […] Kisa cha “Stela” wake nimekisoma kama nasoma riwaya moja kali mno ya mapenzi na mahaba. Bonyeza hapa ukisome. Halafu kaweka picha za “Stela” wakekwenye flickr. We! Brazili tutaenda wote, […]

  9. simbadeo said

    Sankofa,

    Asante sana kwa kisa hiki kitamu. Ni kitamu kwelikweli. Du, akina ‘Stella’ wetu ni wengi. Lakini naamini kuwa Wangui wako bado ni wako hata kama miili yenu haizungumzi lugha moja. Usiache kwenda Brazil.

    Hongera sana. Natamani ungekiandikia kitabu na kisha utuletee kule Mkuki na Nyota huenda kikachapishwa.

    Kila la kheri.

  10. jennifer mhando said

    jamani mbona ni akina stella tu? nasi tuna akina michael wetu! wa kati mwingine nitawasimulia

  11. Jennifer huwezi kuamini ni kwa jinsi gani niko na hamu ya kusikia kisa chako na bwana Michael

  12. […] akina Maiko (Michael)! Kumbe, Da Mija, Serina, Miriam, Shamimu…ninyi akina Michael wenu vipi? Bonyeza hapa umsome dada Jeni akiahidi kutupa kisa cha “Michael” wake. […]

  13. […] kwa kutajwatajwa. Dada Jeni alituuliza hivi karibu, “Mbona Stela tu? Je Michael?” Basi akaahidi kutusimulia ukifika wakati wake. Hapo chini ni kisa cha dada Jennifer Mhando na “Michael” wake (kama […]

  14. […] wa Kitanzania katika kuelezea huko walikopita. Nimeona “Stela” wa Ndesanjo, Luihamu na mimi mwenyewe nikaelezea kuhusu “Stela” wangu, nasikia Simon nae karusha wake, sijacheki bado. Lakini […]

  15. chediel said

    ooh lalaa Safi sana Mkuu ukizinagatia kuanzia sasa utaanza kuapply uparezz ili kwenda Brazil.Nikutakie safari njema.
    Kisa safi sana hicho.

  16. haki Blog said

    h a haha’ bob’ huwezi amini nimepata ombi
    kutoka kwa malkia wa roho yangu kwamba
    nipitie ukurasa huuu niweze soma kama si kusikia
    ulichokiandika kwa ufanisi wa hali ya juu kuhusu mrembo
    Wangui wa Kimari..,
    najuta kuchelewa kupita hawa kwa wakatii,
    kumbuka, historia daima huwekwa na mashujaa…

Leave a reply to luihamu Cancel reply